Mboga za majani ni aina ya chakula ambayo ni muhimu sana katika kuimarisha na kujenga miili yetu
Lakini je , upikaji wetu ni sahihi ?
Zifuatazo ni njia mbalimbali zinazosaidia katika utunzaji na namna ya kuzipika ili kuweza kutunza na kupata virutubisho vyake muhimu katika kujenga miili yetu.
UTUNZAJI WAKE
Nunua mboga mboga na matunda kadiri ya uhitaji wako na uzipike hapo hapo au ndani ya siku mbili ,Utunzaji wa muda mrefu wa mboga za majani hupoteza virutubisho vingi vilivyomo na vyenye umuhimu ndani yake,epuka kuzinunua kwa wingi na kuishia kuzitunza kwa muda mrefu.
Inapotokea umenunua mboga mboga na matunda mengi, basi weka kwenye jokofu la barafu lenye nyuzi 4 au chini ya hapo ili kuweza kutunza virutubisho vyake vya muhimu.
Vile vile pendelea kutunza vyakula kwenye sehemu ya giza na ubaridi kwani vyakula vingi hupoteza virutubisho vyake vinapokaa kwenye sehemu za mwanga na joto.
UANDAAJI WAKE
Osha mboga mboga na matunda yako kwa maji yanayotiririka kama kwenye bomba ili kuweza kutoa vijidudu vinavyoweza kuleta madhara kwenye afya zetu,hivyo epuka kuziloweka kwenye chombo kwani baadhi ya vitamini hupotea kwa njia ya maji.
Pia epuka kumenya maganda ya mboga mboga na hata matunda kwani maganda yake ndiyo yenye virutubisho vingi kuliko hata tunda lenyewe
NAMNA YA KUPIKA
Chagua njia ambazo zitatunza virutubisho vilivyomo kwenye mboga mboga zako ambazo hazitumii moto mwingi utakao ua na kupoteza virutubisho vya muhimu. Hivyo tumia njia ya kupika kama kwa kutumia mvuke kwani hutumia moto kidogo na hata rangi ya mboga haibadiliki na hukufanya kuweza kupata na kutunza virutubisho vyote
Vile vile ni vizuri uzipike bila kukata kata , kwani unapokata unazidi kuongeza uwezekano wa kupoteza virutubisho muhimu.
Pasha moto mboga zako pale ambapo unauhitaji tu, epuka kupasha mara kwa mara ili kuweza kutunza virutubisho vilivyomo kwenye mboga zako.
0 Comments